Kwanza ningependa kumpongeza aliyependekeza kuwa na Jumakiswahili (yaani siku ya kiswahili kama vile Jumamosi ni siku ya kwanza, Jumapili na kadhalika) kwa mtandao wa mawasiliano kwa jina “Twitter”. Ni pendekezo hili lilinifanya niamue kuandika chapisho hili kwa lugha ya taifa ya Kiswahili. Shujaa ni mtu mashuhuri katika jambo; bingwa, shupavu, mshindi, stadi kwa jambo ama mtu ambaye alifanya jambo ambalo linatambulika na watu fulani kama kitendo cha kupewa sifa. Ni kwa sababu hii siku ya Mashujaa imefanywa kuwa siku kuu. Nami leo ningependa kuwatambua baadhi yao na kuwapa heshima wanayostahili.
Ee Mungu nguvu yetu
Ilete baraka kwetu
Haki iwe ngao na mlinzi
Natukae na undugu
Amani na uhuru
Raha tupate na ustawi.
Kwanza, nitaanza na mashujaa ambao walikuwa hai wakati nchi hii yetu ilikuwa inapigania uhuru ambao tunaosherehekea sasa na kuishi, wakati mwingine bila kukumbuka kuwa wakati mmoja hapo kale haukuwa!
Kuna wale wajulikanao sana kama Bildad Kaggia, Kungu Karumba, Fred Kubai, Paul Ngei na Achieng’ Oneko ambao waliwekwa gerezani na rais wa kwanza wa Kenya ambaye sitamtaja hapa kwa sababu ametambulika sana. Sura yake iko kwa hela zetu, mwanawe ako serikalini, ana mali (na mashamba!!) kila mahali – nadhani amepata heshima ya kutosha!! Dedan kimathi Waciuri kwa ujasiri wake na kuifia nchi hii. Sitawasahau akina Tom Mboya, MAU MAU na wengine wengi waliopigania uhuru wetu lakini hawajapata kutambulika. ASANTENI!
Amkeni ndugu zetu
Tufanye sote bidii
Nasi tujitoe kwa nguvu
Nchi yetu ya Kenya
Tunayoipenda
Tuwe tayari kuilinda
Evans Wadongo CNN Hero kwa kuchukua jukumu la kufanya mabadiliko mahala aishipo na mahala usaidizi unahitajika bila ya kumtegemea ‘mheshimiwa’ fulani. Ngugi Wa Thiongo kwa kusimama wima akitetea anachokiamini hata baada ya kutiwa gerezani. David Rudisha kwa kutuonyesha kuwa hakuna rekodi ambayo haiwezi kuvunjwa tena na tena! Timu ya raga kwa jina linalofaa la Shujaa pia ni lazima niwataje kwa kuweza kuipa Kenya sifa zinazoenea hadi kona zote za dunia hii!
Kimani Maruge kwa kutukumbusha kuwa umri si jambo la kumzuia yeyote yule kufanya kile atakalo kulifanya na ana nia ya kuifanya! Maulana aiweke roho yake mahali pema peponi!
Kwa mashujaa wengine kama Wangari Maathai, John Githongo na wengine wengi tutazidi kuwapa heshima wanazostahili na kuwaunga mkono panapohitajika. Mashujaa wa Kenya ya leo ni wengi lakini nimetaja hao kadhaa tu. ASANTENI! Natujenge taifa letu
Ee, ndio wajibu wetu
Kenya istahili heshima
Tuungane mikono Pamoja kazini
Kila siku tuwe na shukrani Shujaa nitakao wataja sasa ni wewe na mimi yaani Wakenya kwa jumla! Mtu yeyote yule anayejitambua kuwa Mkenya ni shujaa! Mengi tumeyaona na kuyapitia; mengi tumevumilia na kujivunia; mengi tungependa hayangetendeka lakini yalitendeka lakini bado tupo wima. Hata baada ya maovu ya watu fulani, bado tulijitokeza kwa wingi kuipigia kura katiba iliyopendekezwa na hata ingawa kulikuwa na tofauti ya maoni kuihusu katiba hiyo, hapakuwa na uhasama!! Kwa sababu hiyo.. kama wewe ni MKENYA,WEWE NI SHUJAA!! Heko kwako!
Kwa hivyo kama wewe wajivunia kuwa Mkenya..jipongeze na uedelee kujivunia!
- Hii ni kazi ya WordTracer(www.twitter.com/Wordtracer) pata picha hii ya kuweka kwa kompyuta yako kwa kuailisha picha (clicking on picture)
Find more writings by Alffie here